Friday 24 April 2015

Tunaweza kuzuia ukatili kwa wanafunzi?


Kushughulika na ukatili wa kijinsia kunajumuisha kufanya mambo mbalimbali na aghalabu yanayochanganya. Hebu kitafakari kisa hiki.

Msichana wa shule mkorofi anabishana na walimu wake na hataki kujiona yuko sawa kama wasichana wengine darasani. Anapokosea anakataa kuadhibiwa.

Kwa upande mwingine, ndani ya darasa hilo hilo kuna msichana anayeonekana mpweke, anajitenga na wenzake na hajiamini.

Mwalimu Grace Nashon wa Shule ya Msingi, Ronsoti iliyopo wilayani Tarime, Mkoa wa Mara anasema kuwapo kwa msichana mkorofi kama huyu darasani, kuna dalili ya asilimia 90 kuwa atakuwa amefanyiwa tohara katika siku za karibuni.

Hali halisi wilayani Tarime
Ukweli ulivyo ni kuwa walimu kama Grace wanakutana na wanafunzi wa aina hizi mara nyingi. Na wanasema kushughulikia ukatili wa kijinsia ni kama kujaribu kupita kwenye njia yenye milima na mabonde ya imani za kiutamaduni.

Kwao haitoshi tu kumkamata mshukiwa wa uonevu huu na kumpeleka akakabiliane na matakwa ya kisheria.

Grace na mwenzake Josephine Hoja,  si tu ni waangalizi wa tabia za watoto shuleni hapo, lakini huwatafuta na kuwapa ushauri na unasihi wasichana na wavulana wanaozongwa na matatizo ya kijamii na kisaikolojia. 

Pamoja na miongo kadhaa ya kazi za ushawishi dhidi ya mila zilizojaa ukatili wa kijinsia kama ukeketaji, mila hii bado inaendelea kufanyika katika Wilaya ya Tarime na kwingineko nchini.

Vitendo vya ukeketaji vinaonyesha kupungua kidogo kutoka asilimia 18 mwaka 1996 hadi 15 mwaka 2010. Hii ni kwa mujibu wa utafiti wa sensa ya watu na afya ya mwaka 2010. Maendeleo haya ni kidogo hivyo kwa jumla ukatili wa kijinsia bado uko juu nchini.

Takribani asilimia 45 ya wanawake waliohojiwa wakati wa sensa hiyo, walikiri kufanyiwa ukatili kimwili na kijinsia katika kipindi fulani maishani mwao.

Hata utafiti mahsusi wa ukatili dhidi ya watoto ulioasisiwa na Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto mwaka 2011, ulionyesha dhahiri jinsi watoto walivyo hatarini kuangukia katika ukatili.

Utafiti unabainisha kuwa, msichana mmoja kati ya watatu na mvulana mmoja kati ya saba ameshawahi kufanyiwa ukatili wa kijinsia. Pia zaidi ya asilimia 70 ya wavulana na wasichana wameshawahi kufanyiwa ukatili wa namna fulani kwenye miili yao kabla ya kutimiza miaka 18.

Kwa uzoefu alionao mwalimu Grace, mara nyingi anapowahisi wanafunzi kuwa na tabia fulani kwa sababu tu walifanyiwa ukatili, hisia hizo huwa kweli.

Kwa mfano, anasema ukimuona mtoto wa kike katika jamii ya watu wa Tarime anajikweza ghafla na kuanza kudharau wakubwa, hali hiyo inatokana na kufanyiwa tohara.

Ukweli ni kuwa kwa upande wa wasichana wenye utayari wa kufanyiwa ukeketaji, kujikweza ni namna ya kuonyesha madai yao ya kupata heshima ya juu zaidi, ambayo kimsingi ni zawadi ambayo jamii huwaandalia wanapotekeleza kitendo hicho cha ajabu.

“Wanawadharau wenzao waliokimbia tohara huku wakionyesha kwamba wao sasa, wamekuwa kundi moja na wanawake wa rika la juu,” anasema mwalimu Josephine.

Mila ya kitumwa
Ahadi za kuingia rika la utu uzima zikiunganishwa na zawadi za vitu mbalimbali, zimewafanya wasichana kukubali miili yao kupitia maumivu makali.

Mila hii ndiyo inayowapa alama ya utumwa wao kwa kila aina ya uonevu wa kijinsia. Ila wasichokijua ni kuwa uonevu wa kijinsia, haushii kwa kukeketwa ni zaidi ya hapo.

Katika jamii zinazoendekeza ukeketaji, wanawake wanamilikiwa na wanaume. Wanageuzwa nguvukazi ya uzalishaji mali, huku wanaume wakimiliki mtaji na faida.

Kwa vile baadhi ya jamii zimelelewa kuona ukeketaji kama kitu bora, waathirika watarajiwa kama yule msichana mkorofi darasani, wanaonekana kuichagua na kuikumbatia mila hiyo.

Kisa cha mwanafunzi mpweke
Kuhusu kisa cha mwanafunzi mpweke, mwalimu Grace anasema alianza kuwa na mwenekano huo baada ya kupotea kwa muda wa wiki mbili.

“Kabla ya hapo alikuwa mcheshi, anayependa kuuliza maswali na anayependa kujieleza mbele ya wenzake,” anamwelezea alivyokuwa awali.

Alipomfuatilia, aligundua kuwa msichana huyo alilazimishwa kukeketwa, kinyume na matakwa yake.

Dosari shuleni
Mojawapo ya sababu za wasichana wanaotaka kukwepa tohara kukosa msaada wa haraka, ni kuwa majukumu ya mwalimu wa malezi shuleni yaliwekwa kwa mtazamo wa kupambana na mimba pekee.

“Tunatumia muda zaidi kupambana na mimba za utotoni kuliko kitu chochote, na hii ni kwa sababu ndivyo maelekezo yanavyosema,” anasema Grace.

Kwa maneno mengine, muda anaotumia mwalimu huyu kutoa ushauri na unasihi kwa watoto wenye shida za kisaikolojia zinazotokana na ukeketaji, hauwezi kuonekana kwenye taarifa zake za utendaji, kwa kuwa si kipaumbele cha kazi yake.

“Umefika wakati sasa, shule na mfumo wa elimu kwa jumla utambue kazi zinazofanywa na walimu kupunguza ama kuzuia athari za mila kandamizi,” anasema Meneja wa mradi wa kupinga ukatili wa kijinsia wa IntraHealth International, huko Tarime, Msafiri Swai.

“Tumeamua kuingia shuleni ili kupanua kazi zetu dhidi ya ukatili wa kijinsia. Shule ni muhimu kwa kuwa ni mazingira ambayo watoto wanaweza kuelimishwa, kuchukia uonevu tangu wakiwa vijana,’’ anaeleza.

Elimu hii na hatimaye matokeo chanya ndiyo ndoto ya wadau wa maendeleo, lakini je, mazingira na mfumo wa elimu unatambua kuwa ukeketaji na ukatili mwingine wa kijinsia ni tatizo? Je, mfumo unatambua kazi ya walimu kama Grace na Josephine shuleni?

Na Mkama Mwijarubi ,Mwananchi

No comments:

Post a Comment

Comment here.....